Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake alioutoa kutokana na mnasaba wa Wiki ya Basij, amesisitiza kwamba: «Bila shaka, sambamba na mwamko wa taifa kubwa la Iran katika kipindi cha Ulinzi Mtakatifu wa Tatu, ambao kwa namna fulani unahesabika kuwa ni kuenea roho ya Basij katika maeneo yote ya nchi, Shirika la Basij nalo linapaswa kufanyiwa mabadiliko na kuzaliwa upya. Shirika hili linapaswa kutumia fursa ya taifa lililoamka kwa kuandaa na kusimamia matoleo mapya na yaliyoendelea zaidi ya Basij ya awali. Hivyo, kuanzia sasa, ni lazima kupiga hatua kubwa, imara na zilizopangwa kwa umakini kuelekea katika utekelezaji wa kaulimbiu ya “Kila Muirani awe mwanachama wa Basij”.»
Hapa chini ni matini kamili ya ujumbe huo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Wiki ya Basij ni fursa mwafaka ya kuitazama upya taasisi hii ya ajabu na yenye thamani kubwa, yaani Basij. Taasisi hii iliyoanzishwa kwa ubunifu na juhudi za Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu alitukuze daraja lake), kwa lengo la kuwakusanya pamoja Wairani wenye ari kubwa, matumaini, kujitolea, wanaotamani heshima ya Uislamu na Iran, pamoja na wale waliojisalimisha kwenye mafundisho ya madhehebu ya Imam Hussein (as), kutoka katika vizazi mbalimbali, hatua kwa hatua na katika kipindi cha maendeleo yake ya kimabadiliko; ili wawe kiini imara cha watu wanaoiunga mkono haki na uadilifu.
Hapo awali, Basij ilijidhihirisha katika kipindi cha miaka minane ya Ulinzi; wakati ilipokuwa na mchango mkubwa katika medani za mapambano ya kijeshi na kuwa tegemeo kuu na mhimili wa vita. Katika kipindi chote cha mapambano hayo matukufu, wanachama wa Basij, kuanzia vijana wadogo hadi wazee, walikuwa wakinufaika kwa manufaa mengi ya kiroho kutokana na mazingira ya kiroho yaliyokuwepo katika mistari ya mbele ya mapambano na mahandaki ya kivita. Kupitia kwao, mazingira ya miji na vijiji vya nchini yalijawa na harufu nzuri ya kiroho.
Kwa namna hiyo, taswira iliyojengeka katika fikra za watu kuhusu Basij na wanachama wake ilikuwa ni taswira ya imani, uwajibikaji, moyo safi, ikhlasi, utambuzi sahihi, ushujaa, jihadi, kutekeleza wajibu na kujitolea kwa ajili ya wengine. Hizi zilikuwa ni sifa zilizokusanyika pamoja, ambazo katika maandiko ya kale ya nchi hii, baadhi yake zilikuwa zikielezwa kuwa ni sifa za mashujaa mashuhuri waliokuwa na maadili mema.
Ikiwa hapo awali baadhi ya wahusika wa simulizi za kubuni na hekaya walikuwa alama za baadhi ya sifa hizi, basi sasa, kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu, wahusika hao wa kweli walikuwa wakitengeneza mashujaa katika simulizi halisi za maisha, wakiwa wamevaa vazi la Basij na kuonesha mifano mingi ya kujitolea.
Ingawa kipindi cha Ulinzi Mtakatifu kilifikia mwisho wake wa heshima baada ya miaka nane, lakini kupitia roho ya Basij, kiliacha athari kubwa katika nyanja mbalimbali za mifumo rasmi na hasa isiyo rasmi ya nchi.
Roho hii ilikuwa ni utajiri mkubwa uliozalishwa na Ulinzi Mtakatifu, mwongozo wa Imam Khomeini (ra), pamoja na uungaji mkono wa makundi makubwa ya wananchi.
Sasa, kwa ajili ya kufafanua zaidi baadhi ya vipengele vinavyokusudiwa katika maelezo haya, ninawasilisha mambo kadhaa yafuatayo:
Kwanza: Bila shaka, sambamba na mwamko wa taifa kubwa la Iran katika kipindi cha Ulinzi Mtakatifu wa Tatu, ambao kwa namna fulani unahesabika kuwa ni kuenea kwa roho ya Basij katika maeneo yote ya nchi, Shirika la Basij nalo linapaswa kupitia mabadiliko na kuzaliwa upya.
Shirika hili linapaswa kutumia fursa ya taifa lililoamka kwa kuandaa na kusimamia matoleo mapya na yaliyoendelea zaidi ya Basij ya awali. Hivyo, kuanzia sasa, ni lazima kupiga hatua kubwa, imara na zilizopangwa kwa umakini kuelekea katika utekelezaji wa kaulimbiu ya «Kila Muirani awe mwanachama wa Basij».
Kwa sasa, wanajeshi wengi wa Jeshi la Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah), vikosi vya ulinzi na usalama, watumishi wa serikali, wabunge na wengineo, kama ilivyo kwa umati mkubwa wa wananchi, kwa sababu mioyo yao imefungamana na mafundisho na mwenendo wa Basij, wanajiona kuwa ni miongoni mwa wanachama wa Basij.
Vivyo hivyo, wafuasi wa bendera waliokuwa wakishikilia bendera katika viwanja na mitaa usiku na mchana, ambao waliupa mwamko wa taifa maana inayoonekana na kugusika zaidi, pamoja na umati mkubwa wa watu waliojitoa mhanga, kwa hakika nao ni miongoni mwao.
Wapo watu wengi ambao si wanachama wa Basij kwa maana ya kawaida ya neno hilo, lakini wanathamini fikra na mafundisho ya Basij na wakati mwingine hulinganisha mwenendo wao na mafundisho hayo. Shirika la Basij linapaswa kutumia kwa namna bora kabisa neema hii waliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
Pili: Mbali na uwezo huo uliopatikana kama ilivyoelezwa hapo juu, Shirika rasmi la Basij linapaswa daima kujitahidi kueneza roho ya Basij katika kila sehemu ya nchi.
Roho ya Basij, ambayo baadhi ya sifa zake zimeelezwa hapo awali, inaweza kuenezwa katika sehemu mbalimbali za jamii kupitia mwenendo na tabia za wanachama wenyewe wa Basij.
Kufuata tabia njema, huruma na upole, kuwaheshimu wananchi, kuzingatia nyanja mbalimbali za uchamungu wa mtu binafsi na wa kijamii, pamoja na kudumisha mwenendo ambao wanachama wengi wa Basij walikuwa wakitambulika nao tangu nyakati zilizopita, kama vile unyenyekevu, kujishusha, kujitolea, kutopenda kujionesha mbele ya watu, kujiepusha na anasa na mambo ya kifahari, pamoja na tabia nyingine nzuri za aina hii, kutawafanya wanachama hao kuwa nuru na fahari ya wananchi katika kila mtaa, mji na kijiji. Aidha, kutawafanya watu wote kuvutiwa na kuiga mwenendo na njia hiyo ya maisha.
Tatu: Msingi mkuu wa kujifungamanisha wanachama wa Basij ni mafundisho ya madhehebu ya Imam Hussein (as), ambayo ndiyo tafsiri sahihi ya Uislamu halisi wa Muhammad (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Ahlul-Bayt wake).
Kila aina ya kujenga uhusiano au kujitenga, pamoja na kila aina ya kumpenda mtu au kujitenga naye, kwa wanachama hao hujengwa kwa msingi huu.
Mafundisho mawili yenye kuhuisha maisha kutoka katika Qur'ani Tukufu, ambayo ni: «Wao ni wenye kuhurumiana wao kwa wao» na «Wao ni wakali dhidi ya makafiri», ndiyo mwanga unaoongoza nyoyo za wanachama wa Basij.
Kwa msingi huo, wao huonesha huruma na kujitolea kwa wananchi, mfumo wa Kiislamu na Mapinduzi ya Kiislamu. Vilevile, hawapotezi fursa yoyote ya kuwadhuru maadui wa Uislamu na mfumo wa Kiislamu.
Kulinda mshikamano wa kijamii na umoja mtakatifu wa taifa la Iran, ambao katika siku hizi thamani yake kubwa na athari zake za ajabu katika kuendeleza ushindi wa wapiganaji jasiri na wenye kujitolea wa Uislamu katika medani za kijeshi dhidi ya mfumo wa mahesabu ya adui, katika pande zote mbili za uwanja wa mapambano kati ya haki na batili, ni mambo yaliyo wazi na yanayoonekana; kunapaswa kuwa miongoni mwa sifa za pamoja za wanachama wote wa Basij.
Nne: Kwa msaada wa wanachama wake, Basij imekuwa ikiziba mapungufu mengi ya taasisi rasmi na zisizo rasmi katika kipindi chote cha uwepo wake hadi sasa.
Sasa, kwa kuzingatia ukuaji mkubwa wa Basij katika kipindi cha mwamko wa wananchi wa Iran, uwezo uliopo na watu wote wanaohesabika kuwa wanachama wa Basij kwa dhati ya mioyo yao, wakiwemo wale waliokuwa katika viwanja na mitaa, waliojitolea, pamoja na wengine ambao wameungana nao katika ahadi ya pamoja ya kufikia ukamilifu wa mtu binafsi na wa kijamii; watu ambao nyoyo zao ndizo zinazohesabika kuwa makao halisi ya Basij, wote hao wanaunda nguvu kubwa sana.
Nguvu hii inapaswa kutumika kikamilifu, kipengele baada ya kingine, katika njia ya kutatua matatizo ya nchi na kufikia fursa mpya na za kipekee. Kwa namna hii, kaulimbiu ya «Kila Muirani awe mwanachama wa Basij» itapewa maudhui na uzito mkubwa zaidi.
Inatarajiwa kwamba, kwa kuzingatia mambo haya, Basij ya Wairani itaweka katika historia ya nchi hii mfano bora na wa hali ya juu wa kusaidiana, pamoja na kiwango cha juu cha utekelezaji wa dhana ya Umma na Taifa; kiasi kwamba jambo hilo litakuwa mwanzo wa maendeleo na mafanikio makubwa yatakayopatikana katika siku zijazo.
Ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awajalie mashahidi wetu wapendwa wa Basij neema ya Ridhaa Yake na kuishi jirani na Ahlul-Bayt (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote). Pia, ninamwomba awajalie maveterani wetu wapendwa wenye majeraha ya vita subira na afya njema, na awaweke Wabasiij wote wa Iran pamoja na wale wa Muqawama, ambao mimi ni mmoja wa wanachama wao wadogo kabisa, miongoni mwa askari wa Bwana wetu (Imam Mahdi), Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake. Aidha, awajaalie wawe miongoni mwa wanaonufaika na dua zake njema, ushindi na baraka zake.
Sayyid Mujtaba Husseini Khamenei
Maoni yako